Hatimaye Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), imeibuka na kueleza wazi
kuwa dawa pekee zinazofaa ni zile zilizothibitishwa kitaalamu kuwa
zinafaa kwa matibabu hayo na siyo vinginevyo.
Kuwapo kwa utitiri wa matangazo holela ya dawa za nguvu za kiume,
hasa katika maeneo ya mijini ikiwamo jijini Dar es Salaam na ndio
kulisababisha kuweo kwa nia ya kutambua dawa rasmi zilizothibitishwa na
TFDA na wala hazizidi tano.
Nyingine nyingi hazijathibitishwa na hivyo kuwa na uwezekano wa
kutotimiza matarajio ya watumiaji au kuwahatarisha na madhara
mbalimbali, yakiwamo ya kupasuka kwa mishipa ya damu iliyopo kwenye
moyo.
Afisa Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza, alisema kwamba, ni kweli
kuna dawa nyingi zinazotangazwa na watu mbalimbali kuwa zinatibu tatizo
la nguvu za kiume, lakini zilizo rasmi ni pamoja na Viagra, Erecto, Cialis na Suagra.
Simwanza alisema dawa hizo ndizo wanazozitambua kuwa zinaweza
kutumiwa na watu waliopungukiwa au kuishiwa kabisa nguvu za kiume, kwa
sababu zimepitishwa baada ya kukidhi vigezo vya kitaalamu. Hata hivyo,
Simwanza alisema dawa hizo siyo za kutumiwa kiholela bali wenye shida
nazo ni lazima wafuate maelekezo ya madaktari ili kujiepusha na madhara
yake pindi zikitumika kiholela.
“Kuna dawa nyingi ambazo sisi tunazitambua na tumezipitisha zitumike,
lakini mtu asizitumie hadi pale atakapopewa ushauri wa daktari. Hizi
zina nguvu sana na zinaweza kufanya mishipa ya moyo kupasuka ama
kuathiri mfumo wa damu kwa watu wanaozitumia bila kufuata maelekezo ya
madaktari,” alisema Simwanza.
Alipoulizwa kuhusu dawa za asili za kuongeza nguvu za kiume, zikiwamo
maarufu za kizizi cha mkuyati na zile zinazofahamika kama vumbi la
Kongo, zikihusisha orodha ya dawa mbalimbali za aina hiyo kutoka Kongo
zikiwamo za kasongo na mundende, Simwanza alisema TFDA hawawezi
kuzizungumzia hizo na badala yake waulizwe wataalamu wa kitengo cha Tiba
Asili na Tiba Mbadala cha Wizara ya Afya.
Dawa nyingine maarufu za kiasili ambazo huuzwa katika maeneo
mbalimbali jijini Dar es Salaam, hutambulishwa kwa majina ya mkongoraa,
sheki na oljanilolo inayopatikana zaidi kwa morani wa Kimasai.
Alipoulizwa kuhusu dawa hizo za asili kwa ajili ya kushughulikia
tatizo la nguvu za kiume, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili na
Tiba Mbadala katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Paul Mhame,
alisema hivi sasa Wizara ya Afya iko katika utaratibu wa kusajili dawa
za asili zikiwamo hizo (kizizi cha Mkuyati na jamii ya vumbi la Kongo)
ikiwa zitathibitika kuwa zinafaa na hazina madhara kwa watumiaji.
Akieleza zaidi, Dk. Mhame alisema kuwa hadi sasa hakuna dawa ya asili
yoyote ambayo imesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na
kwamba, kwa sababu hiyo, hakuna dawa ya kiasili ambayo Wizara inaweza
kuizungumzia kwa uwazi kuwa imethibitishwa kuwa inaongeza nguvu za kiume
pasi na kuwa na madhara yoyote kwa watumiaji.
Dk. Mhame aliongeza kuwa kwa sababu hiyo ya kutokuwapo kwa usajili
rasmi kwa dawa za asili hadi kufikia sasa, ni vyema watumiaji wakawa
waangalifu kutumia dawa za namna ya kizizi cha Mkuyati na vumbi la Kongo
zinazouzwa kiholela mitaani kwa sababu zinaweza kuwasababishia madhara
makubwa kiafya kwa vile ni dawa ambazo hazina vipimo sahihi vya matumizi
yake.
Hata hivyo, Dk.Mhame alikiri kuwa Tanzania ina miti mingi ya asili
ambayo inaweza kutumika kutibu masuala ya tendo la ndoa baina ya
wapendanao, lakini ni muhimu kutambua kuwa tiba inapotangazwa kwa sura
ya kibiashara inatia shaka na hivyo watumiaji wanapaswa kuwa macho.
“Kwa mfano, kuna watu wanauziwa kile wanachoelezwa kuwa ni supu ya
pweza mitaani kuboresha afya zao hasa kuhusu nguvu za kiume… lakini ni
muhimu kuwa waangalifu ili kujiridhisha kuwa kweli kinachouzwa na watu
kunywa ni supu ya pweza au ni maji tu ya kawaida,” alitahadharisha Dk.
Mhame.
Aliongeza kuwa zipo dawa kadhaa za tiba asili ambazo baraza
wanazitambua kuwa husaidia kutatua tatizo la nguvu za kiume, lakini
nyingi hazifanyi kazi za papo kwa papo kama watu wanavyoaminishwa, bali
nyingi humlazimu mhusika atumie dawa hizo kwa siku akdhaa ili mwili
urudi katika hali yake ya awali na kupata jawabu ya kile
kinachotarajiwa.
Alisema kuwa, ipo mimea imethibitika pia kutatua tatizo la nguvu za
kiume kama mahama au mapama, ubuyu na majani ya mlonge, lakini zote hizo
humsaidia mtu aliyepungukiwa na nguvu za kiume kurudisha mwili wake
katika hali ya kawaida baada ya dawa hizo kutumiwa kwa siku kadhaa na
siyo papo kwa papo, kama inavyoelezwa kuhusu kizizi cha mkuyati na vumbi
la Kongo.
Aliongeza kwa kusema, ili dawa ya tiba asili ifanye kazi papo kwa
papo, ni lazima ikamuliwe na kuondolewa viambata vingine ndipo itafanya
kazi papo kwa papo kama ilivyo kwa dawa aina ya Viagra, lakini muhimu ni
kufuata maelekezo ya daktari. Upset couple finding out results of a pregnancy test
No comments:
Post a Comment