
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameviomba vyama vya Chadema na CCM kusimamisha kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani kwa siku tatu kuomboleza kifo cha mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru.
Zitto ameyasema hayo leo Februari 3, mwaka huu akiwa katika msiba wa mwanasiasa huyo, nyumbani kwake Kijitonyama, Dar es Salaam.
“Kingunge amesaidia kuimarisha CCM na baadaye akasaidia Chadema. Sioni busara vyama kuendelea na kampeni. Nawaomba wasitishe leo, kesho na Jumatatu mwanasiasa huyu akizikwa wataendelea,” amesema Zitto.
Vyama takribani 12 vipo katika kampeni za ubunge jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro. Kampeni hizo zilianza Januari 21 na kutarajiwa kumalizika Februari 16. Uchaguzi katika majimbo hayo na Kata 10 utafanyika Februari 17, 2018.
Mwanasiasa huyo alifariki dunia jana Februari 2, 2018 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), anatarajiwa kuzikwa Jumatatu Februari 5, 2018 katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment