Rais wa Gabon Ali Bongo anarejea
nchini mwake leo Jumanne baada ya kuwa nje ya nchi kwa zaidi ya miezi
miwili akipokea matibabu nchini Morocco.
Bw Bongo anarejea wiki moja tu baada ya jeshi nchini humo kufanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi ya serikali yake.Kiongozi huyo mwenye miaka 59 amekuwa akipokea matibabu nchini Morocco tangu Oktoba 24 alipopata kiharisi akihudhuria mkutano mkuu wa kiuchumi nchini Saudi Arabia.
Baada ya utata kuhusu hali yake, makamu wake hatimaye alitangaza mwezi Desemba kwamba alipatwa na kiharusi.
Mara pekee kwake kuonekana na umma ilikuwa ni wakati wa hotuba ya kila mwaka ya Mkesha wa Mwaka Mpya ambayo ilirekodiwa akiwa Morocco.
Alieleza kwamba alikuwa amepitia "wakati mgumu."
Wakosoaji wake walitumia hali kwamba alionekana dhaifu na sauti yake kutokuwa na nguvu sana kueleza kuwa hali haikuwa shwari.
Wiki iliyopita, jeshi nchini humo lilizima jaribio la mapinduzi ya serikali na kumkamata kiongozi wa kundi hilo na pia kuwaua wanajeshi wawili waliokuwa wamevamia kituo cha redio ya taifa.
Wanajeshi hao walisema walihisi hotuba ya Bw Bongo ya Mwaka ilidhihirisha kwamba kiongozi huyo alikuwa amepoteza uwezo wake wa kuliongoza taifa hilo.
Mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu Julien Nkoghe Bekale alitangaza mabadiliko katika baraza la mawaziri.
Katiba ya Gabon inasema mawaziri ni lazima wale kiapo mbele ya rais
Shirika la habari la Reuters hata hivyo linaripoti kuwa wanahabari hawataruhusiwa kuhudhuria hafla hiyo.
Familia ya Bongo imetawala taifa hilo kwa miaka 51 iliyopita, na imetuhumiwa kwa kujilimbikizia mali na utajiri mkubwa kutokana na rasilimali za taifa hilo.
Rais Ali Bongo alichukua madaraka ya kuiuongoza nchi hiyo kutoka kwa babab yake Omar Bongo mwaka 2009, ambaye aliiiongoza nchi hiyo ya Afrika magharibi kwa zaidi ya miaka 40.
Alishinda uchaguzi wa marudio mwaka 2016, katika zoezi lililotawaliwa na ghasia na tuhuma za udanganyifu.
katika uchaguzi huo, Bw Bongo alipata ushindi kwa 49.8% ya kura naye Bw Jean Ping akapata 48.2 % ya kura, kura zilizowatenganisha zikiwa 5,594.
No comments:
Post a Comment