Thursday, 27 December 2018

Kabwili Aitaka Simba

Kabwili Aitaka Simba
Kipa kinda wa Yanga, Ramadhani Kabwili, amesema anatamani kupangwa katika kikosi kijacho kitakachocheza na Simba ili aweze kuonyesha ubora wake.
Yanga na Simba zinatarajia kukutana Februari 19, mwakani katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kabwili kwa sasa ni kipa namba moja katika kikosi cha Yanga baada ya mkongwe, Beno Kakolanya, kutofautiana na klabu yake hiyo kutokana masilahi anayodai.
Akizungumza nasi jana, Kabwili alisema anahitaji kupata mchezo wenye presha kubwa ili aweze kutambua yuko fiti kiasi gani langoni.
Aidha, kinda huyo alieleza kuwa kama akipangwa katika mechi ya watani dhidi ya Simba ataongeza umakini na kujiamini langoni ili kuwadhibiti washambuliaji wake.
Aliongeza kuwa kikosi hicho cha Msimbazi kina washambuliaji wakali kama Emmanuel Okwi, John Bocco, Meddie Kagere na kiungo mshambuliaji anayefunga mabao, Clatous Chama.
“Mwaka jana nilidaka katika michuano ya kimataifa kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St. Lois ya visiwa vya Shelisheli, sasa hivi natamani mchezo wetu na Simba ili nionyeshe ni jinsi gani nimeiva.
“Nashukuru benchi la ufundi kuniona ninaweza kuibeba timu jambo ambalo limeniongezea ujasiri wa kudaka mechi kubwa,” alieleza Kabwili.

No comments:

Post a Comment