Monday, 28 January 2019

Kwa rekodi hizi Simba ijipange kwa Al Ahly

Mambo mawili makubwa yanaipa Simba wakati mgumu wa kupanda mlima mrefu ili kuibuka na ushindi dhidi ya Al Ahly ugenini, Cairo Misri, Jumamosi wiki hii katika mchezo wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kiwango na matokeo bora ya wapinzani wao kwa sasa pamoja na rekodi mbovu ya Simba ugenini dhidi ya timu kutoka nchi za Kaskazini mwa Afrika, vinaongeza presha kwa wawakilishi hao wa Tanzania kabla kuvaana na Al Ahly.
Ndani ya uwanja, Al Ahly ina kikosi chenye muendelezo wa ubora ambacho kimekuwa kikiisaidia kupata matokeo mazuri kwenye ligi ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Al Ahly ambayo ni tishio kwa mashambulizi ikitokea pembeni mwa eneo la kuchezea, msimu uliopita ilicheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kupoteza mbele ya Esperance ya Tunisia kwa matokeo ya jumla ya mabao 4-3.
Msimu huu hadi sasa inaongoza Kundi D ikiwa na pointi nne, ikifunga mabao matatu na nyavu zao kutikiswa mara moja huku nyuma yao ikiwepo AS Vita ya DR Congo inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu sawa na Simba na JS Saoura inashika mkia.
Mashambulizi ya kupitia pembeni mwa uwanja ambayo Al Ahly imekuwa ikipendelea kufanya, yamekuwa yakichagizwa zaidi na kasi kubwa ambayo timu hiyo imekuwa nayo hasa inaposhambulia au inapotaka kupoka mpira kwa timu pinzani.
Upande wa kushoto wa Al Ahly unapaswa kutazamwa zaidi na Simba kwa kuwa ndio umekuwa tishio zaidi kwa mabeki wa timu pinzani ambao una winga Ramadan Sobhi anayecheza kwa mkopo akitokea Huddersfield inayoshiriki Ligi Kuu ya England lakini pia una beki wa kushoto, Ali Maaloul.
Hata hivyo, Sobhi amekuwa akibadilisha upande mara kwa mara kutokana na ubora na udhaifu wa mabeki wa pembeni wa timu pinzani.
Rekodi za uhakika ambazo gazeti hili linazo, zinaonyesha Simba haijawahi kupata ushindi na imetoka sare mara moja tu ndani ya dakika tisini katika mechi zote ambazo imewahi kucheza ugenini dhidi ya klabu kutoka Arabuni kwenye mashindano ya Klabu Afrika.
Pamoja na rekodi nzuri ya Simba kuzitesa au kutopoteza mechi dhidi ya timu za kiarabu, wawakilishi hao wa Tanzania ni dhaifu pindi wanapokwenda ugenini kukabiliana na klabu zinazotoka ukanda wa Kaskazini.
Katika mashindano mbalimbali ya Afrika kwa ngazi ya klabu, Simba imekutana na timu kutoka mataifa ya kiarabu mara 10 ugenini ambapo kati ya hizo mechi tisa ilipoteza na moja ilitoka sare.
Vipigo vya Simba pindi inapocheza ugenini Arabuni vilianzia mwaka 1974 kwenye hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mehalla Kubra ambapo baada ya kushinda bao 1-0 nyumbani, ilifungwa 1-0 ugenini na kuondoshwa kwa mikwaju ya penalti 3-0.
Mwaka 1993, ilifanikiwa kuwatoa USM El Harrach ya Algeria katika hatua ya robo fainali ya Kombe la CAF, kwa matokeo ya jumla ya mabao 3-2. Simba ilishinda 3-0 nyumbani kabla ya kufungwa 2-0 ugenini.
Matokeo mengine ya Simba ugenini baada ya kufanya vizuri nyumbani ni kufungwa mabao 2-0 na Al- Mokawloon ya Misri mwaka 1996, kufungwa 1-0 na Zamalek ya Misri mwaka 2003, kufungwa 2-1 na Ismailia mwaka 2003, kufungwa 2-0 na Ismailia mwaka 2001, kufungwa 5-1 na Haras El Hodood mwaka 2010, kufungwa 3-0 na Al- Ahyl Shendi mwaka 2012 na pia kufungwa 2-0 ugenini dhidi ya ES Setif.
Mwaka jana Simba ilipata unafuu baada ya kutoka suluhu ya kwanza ikiwa ugenini dhidi ya Al Masry katika mechi ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kocha wa Prisons ya Mbeya, Mohammed ‘Adolph’ Rishard, alisema Simba inapaswa kuongeza kasi katika maandalizi kujiandaa na mchezo huo.
Nyota huyo wa zamani wa Taifa Stars, alisema ingawa Simba haina rekodi nzuri Misri, lakini inaweza kufanya maajabu ugenini kama ilivyofanya dhidi ya Zamalek.
Source : Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment