Wednesday, 2 January 2019

Zahera aishika pabaya Simba

Zahera aishika pabaya Simba
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ni kama amewakamata pabaya Simba baada ya kutamka wazi kwamba wakati huu wapinzani wao hao wakiwa bize na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ndipo pa kuwatimulia vumbi Ligi Kuu.
Simba wametinga hatua ya makundi ligi hiyo ya Mabingwa na wamepangwa kundi D sambamba na AS Vita ya Congo, JS Soura ya Algeria pamoja na mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri.
Michezo ya kwanza ya hatua hiyo ya makundi inatarajiwa kuanza Januari 11 mwaka huu ambapo Simba wataanzia nyumbani dhidi ya JS Soura mchezo utakaochezwa Jumamosi ya Januari 12 Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kutokana na hali hiyo, kocha huyo wa Yanga amesema kwamba, anataka kuhakikisha timu yake inaendelea kutoa dozi na kujikita kileleni kwa kuwa na pointi na mabao mengi, ili Simba watakaporejea katika ligi wawe wameachwa mbali.
“Hapa tunayo michuano mingine ya Mapinduzi lakini akili yangu ipo Ligi Kuu pamoja na FA, nataka tuendelee kujikusanyia pointi wakati huu Simba wakiwa wanashiriki Ligi ya Mabingwa, hatutakiwi kupoteza mchezo wowote.
“Tunatakiwa tuendelee kushinda ili wao wakishamaliza kucheza michezo yao ya kimataifa watukute tupo mbali na pointi za kutosha, naamini hiyo itaweza kutusaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
“Kufuatana na nguvu yetu tulionayo (wachezaji) inatubidi tuangalie wapi tutapata faida, tupo na ligi kuu, tupo na Azam Federation Cup, Mapinduzi Cup na Sport Pesa, inabidi sisi kama Yanga tuwe na malengo kwenye kitu chenye manufaa kwetu tukiamua kuyataka makombe yote tunaweza kukosa yote hivyo lazima baadhi ya wachezaji wapumzike,” alisema.
Yanga itaanza kushuka uwanjani kesho kuwakabili KVZ kwenye michuano ya Mapinduzi, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar ambapo Zahera amesema huenda akawapumzisha baadhi ya wachezaji wake muhimu kwaajili ya Ligi Kuu.
Katika msimamo wa Ligi Kuu, Yanga wanaongoza wakiwana pointi 50 katika michezo 18 waliyocheza wakifuatiwa na Azam wenye pointi 40 wakicheza michezo 17 huku Simba wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 33 wakicheza michezo 14, ambapo Zahera anataka kukalia usukani huo mpaka mwisho.
Source : Dimba

No comments:

Post a Comment