Wednesday, 2 January 2019

Nyota wawili Simba kumfuata Samatta

Nyota wawili Simba kumfuata Samatta
NYOTA wawili wa Simba, Adam Salamba na Paul Bukaba, muda wowote kuanzia sasa wanaweza wakaondoka ndani ya kikosi cha timu hiyo kwenda nchini Ubelgiji kukipiga Ligi Kuu ya nchini humo.
Taarifa kutoka Simba zinadai kwamba kuna moja ya klabu inayoshiriki ligi nchini humo anakocheza Mtanzania Mbwana Samatta, imevutiwa na uwezo wa wachezaji hao na huenda wakala ‘shavu’ la nguvu hivi karibuni.
Kigogo mmoja ndani ya Simba alituambia kuwa, kuna barua pepe imetumwa kutoka Ubelgiji ikitaka pande mbili kukaa meza moja ili kuzungumza namna ya kufanya biashara hiyo.
“Tulipokea barua hiyo kwa njia ya FAX , lakini ilipitia jina la Jamal Kisongo ambaye ni meneja wa wachezaji hao, hebu mtafute nadhani atakuambia nini kinaendelea,” alisema kigogo huyo.
Tulipomtafuta Jamal Kisongo ambaye ni meneja wa wachezaji hao na kukiri kwamba wateja wake wamepata ofa hiyo licha ya kukataa kuitaja timu inayowataka akidai wanafanya mambo yao kimyakimya.
“Ni kweli kuna ofa kutoka Ubelgiji, ila sitaweza kutaja timu kwani bado mambo yapo katika mchakato, hapa nilipo napambana kuhakikisha hadi Januari 10 mwaka huu vijana hao wawe wameshaondoka,” alisema Kisongo.
Kama dili hilo likifanikiwa nyota hao wataungana na nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta anayekipiga katika klabu ya KRC Genk inayoongoza Ligi Kuu nchini humo.

No comments:

Post a Comment